Imarati yawatumia wapiganaji wa Haftar ndege 100 zilizosheheni silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59376-imarati_yawatumia_wapiganaji_wa_haftar_ndege_100_zilizosheheni_silaha
Imebainika kuwa, ndege 100 za mizigo zilizosheheni silaha na zana za kijeshi zimewasili nchini Libya zikitokea Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2020 04:30 UTC
  • Imarati yawatumia wapiganaji wa Haftar ndege 100 zilizosheheni silaha

Imebainika kuwa, ndege 100 za mizigo zilizosheheni silaha na zana za kijeshi zimewasili nchini Libya zikitokea Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Duru za habari zimefichua kuwa, ndege hizo za mizigo kutoka UAE zimekuwa zikiondoka Abu Dhabi  na kwenda mashariki mwa Libya, kwa ajili ya kuwapelekea silaha wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya.

Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa ya Libya imesema kuwa, Imarati imetuma ndege 100 zilizosheheni zana za kijeshi kwa wanamgambo wa Haftar kati ya Januari 12 na Februari 23 mwaka huu 2020. Habari zaidi zinasema kuwa, ndege hizo zilikuwa zimebeba shehena za silaha zinazokadiriwa kuwa na uzani wa tani 6,190.

Kwa mujibu wa taarifa, ndege hizo zilitoka nje ya rada muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Suweihan huko Imarati, na kisha zikaoneka zikitua katika viwanja vya ndege vya jeshi vinavyopatikana mashariki mwa Libya na magharibi mwa Misri.

Wapiganaji wa Haftar wanaoungwa mkono na Imarati, Saudia, Misri na nchi nyinginezo

Ifahamike kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu ni moja ya waungaji mkono wakuu wa jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya katika vita vya kutaka kudhibiti mji mkuu Tripoli tokea Aprili mwaka jana.

Ndege zisizo na rubani (droni) za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zimekuwa zikifanya mashambulizi katika mji wa Misrata wa kaskazini mwa Libya.