Bunge la Tunisia lapasisha serikali mpya ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59419-bunge_la_tunisia_lapasisha_serikali_mpya_ya_nchi_hiyo
Hatimaye na baada ya vuta nikuvute na malumbano makubwa ya kisiasa, Bunge la Tunisia limepasisha serikali mpya ya nchi hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu, Elyes Fakhfakh kwa kura 129 za diyo mkabala wa kura 77 za upinzani. Serikali mpya ya Tunisia imepasishwa baada ya mjadala mkali ulioendelea kwa muda wa masa 14.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2020 07:39 UTC
  • Bunge la Tunisia
    Bunge la Tunisia

Hatimaye na baada ya vuta nikuvute na malumbano makubwa ya kisiasa, Bunge la Tunisia limepasisha serikali mpya ya nchi hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu, Elyes Fakhfakh kwa kura 129 za diyo mkabala wa kura 77 za upinzani. Serikali mpya ya Tunisia imepasishwa baada ya mjadala mkali ulioendelea kwa muda wa masa 14.

Ajenda kuu ya serikali mpya ya Tunisia ni kushughulikia matatizo yanayoizonga nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kupambana na ufisadi, ughali wa bidhaa, uhalifu wa kupanga na kutayarisha nafasi za ajira.

Baada ya serikali yake kupata ridhaa ya Bunge, Waziri Mkuu wa Tunisia Elyes Fakhfakh amesema kuwa: Serikali hii itaamiliana kwa heshima na vyama vyote vya siasa sawa viwe vya upinzani au vyama vinavyoiunga mkono serikali na inanyoosha mkono wa ushirikiano kwa jumuiya na taasisi zote za kitaifa ikiwemo Jumuiya ya Wafanyakazi, wawekezaji na Jumuiya ya Wakulima.

Elyes Fakhfakh akihutubia Bunge la Tunisia

Bunge la Tunisia limepasisha serikali mpya ya nchi hiyo baada ya mkwamo wa kisiasa ulioendelea kwa kipindi cha karibu miezi mitatu. Elyes Fakhfakh, aliyekuwa waziri wa fedha, alipewa jukumu la kuunda serikali mpya ya Tunisia baada ya Bunge kukataa serikali iliyopendekezwa na mtangulizi wake, Habib Jemli, Januari mwaka huu. Fakhfakh ametangaza kuwa serikali yake itatoa kipaumbele kwa suala la kujiepusha na mivutano ya kisiasa na kujikita katika masuala ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi katika nyanja za kiuchumi na kijamii. Awali mipango na ajenda ya Fakhfakh na serikali yake haikukubaliwa na chama cha al-Nahdha ambacho ndicho chenye viti vingi katika Bunge la Tunisia. Upinzani wa al Nahdha dhidi ya ajenda za Fakhfakh uliendeleza mkwamo wa kisiasa wa Tunsia kiasi kwamba, wiki iliyopita Rais wa nchi hiyio, Kais Saied, alitishia kuwa, atalivunja Bunge na kuitisha uchaguzi wa kabla ya wakati kwa mujibu wa kipengee cha 89 cha katiba ya nchi hiyo endapo serikali ya Elyes Fakhfakh itashindwa kupata kura za kuwa na imani nayo. Hatimaye baada ya majadiliano na mazungumzo baina ya vyama vya siasa, chama cha al Nahdha kilikubali kulegeza msimamo wake na kutangaza kuwa, kitashiriki katika serikali mpya ya Tunisia.

Katibu Mkuu wa chama cha al Nahdha, ametoa taarifa akisema: Uamuzi wa kushirikiana na serikali umechukuliwa kwa kutilia maanani mazingira tata na hatari ya kipindi cha sasa hususan vita vya Libya na hali ngumu ya kiuchumi ndani ya Tunisia.   

Rashid al Ghanushi

Matatizo ya kiuchumi hususan ukosefu wa ajira ni miongoni mwa changamoto kubwa za nchi ya Tunisia ambayo imekuwa ikikumbwa na maandamano makubwa na ya mara kwa mara ya wananchi katika miaka ya hivi karibuni. Hali hii, kama wanavyosisitiza wachambuzi wa mambo, ndiyo sababu ya ushiriki mdogo sana wa Watunisia katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana. Takwimu zinaonyesha kuwa, kiwango cha ukosefu wa ajira baina ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 wa Tunisia kimefikia asilimia 30. Hii ni pamoja na kuwa kiwango cha mfumuko wa bei na ughali wa maisha pia kimeongezeka mara dufu ikilinganishwa na kile cha miaka ya 90 kwa kadiri kwamba, familia maskini nchini Tunisia zinashindwa kupata mahitaji ya chakula na mlo wa kila siku au kununua nishati na umeme.

Ni kwa kutilia maanani hali hiyo ndipo Waziri Mkuu mpya wa serikali ya Tunisia akaahidi kushughulikia matatizo ya kiuchumi na kutayarisha nafasi zaidi za ajira, akivitaka vyama vya siasa na maafisa wa serikali kuisaidia serikali yake. Suala jingine ambalo limesisitizwa na Elyes Fakhfakh ni suala la kupambana na ugaidi na wimbi la wahajiri haramu hususan kwa kutilia maanani vita na mapigano ya ndani yanayoendelea katika nchi jirani ya Libya.

Watunisia wanapinga hali mbaya ya uchumi

Katika hali hii wananchi wa Tunisia wanasubiri kuona iwapo serikali mpya itatekeleza kivitendo ahadi zake hususan katika upande wa masuala ya kiuchumi ambayo ndiyo yanayowalemea zaidi wananchi wa kawaida.