Mar 05, 2020 11:21 UTC
  • Mgonjwa wa mwisho Ebola arejea nyumbani DRC

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa mgonjwa wa mwisho wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ameruhisiwa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa matibabu katika kituo cha matibabu huko kaskazini mashariki mwa mji wa Beni.

Taarifa ya WHO iliyotolewa jana mjini Brazzaville Congo na Goma DRC, ilisema kukiwa hakuna kisa kingine chochote kipya kilichothibitika, tangu Machi pili, zimesalia siku 42 kuelekea kabla ya kutangazwa mwisho wa mlipuko wa Ebola, wa pili kwa ukubwa duniani.

Utaratibu uliopo ni kuwa ili kutangaza mwisho wa mlipuko wa ugonjwa ni lazima zipite siku 42 tangu mara ya mwisho mgonjwa wa mwisho alipopimwa na kukutwa bila maambukizi.

Ingawa mgonjwa wa mwisho wa Ebola ameruhusiwa kurejea nyumbani, WHO inasema inaendelea kuwafuatilia kwa karibu sana watu 46 ambao kwa namna moja au nyingine walikutana na mgonjwa huyo kabla ahajapatiwa matibabu.

Chanjo ya Ebola

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt Matshidiso Moeti amesema: “Ninazipongeza juhudi za bila kuchoka ambazo zimefanywa kushughulikia mlipuko huu na ninahamasishwa na taarifa kwamba mgonjwa wa mwisho wa Ebola ameondoka katika kituo cha tiba akiwa mwenye afya njema. Huu siyo mwisho wa Ebola katika DRC. Tunatakiwa kukaa chonjo katika wiki zijazo na kuendelea.”

Mlipuko wa hivi sasa ambao ulitangazwa mnamo tarehe mosi ya mwezi Agosti 2018, ni wa kumi katika nchi ya DRC na wa pili kwa ukubwa kimataifa baada ya ule wa mwaka 2014 hadi 2016 huko Afrika Magharibi. Hadi kufikia tarehe Mosi ya mwezi huu wa Machi, kulikuwa na visa 3, 444 vilivyothibitishwa na vilivyohisiwa kuwa ni ugonjwa huo, huku kukiripotiwa vifo 2, 264.

Bado juhudi za ufuatiliaji, upimaji na utoaji taarifa ikiwemo kushirikiana na mamlaka hadi ngazi ya jamii zinaendelea ili kufuatilia hali katika jamii.

Tags