AU yalaani jaribio la mauaji dhidi ya Waziri Mkuu wa Sudan
Umoja wa Afrika umelaani shambulizi la bomu dhidi ya Waziri Mkuu wa Sudan, Abdulla Hamdok ambaye alinusurika kifo jana kufuatia mlipuko wa bomu uliolenga gari lake katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Afrika imesema Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Moussa Faki Mahamat amelaani vikali shambulizi hilo dhidi ya msafara wa magari ya Waziri Mkuu wa Sudan mjini Khartoum.
Umoja wa Afrika umewahimiza wadau wote waonyesha mshikamano kwa serikali ya mpito ya Sudan na kulinda misingi ya demokrasia nchini humo.
Habari zinasema Hamdok alinusurika kifo jana Jumatatu baada ya msafara wake wa magari kushambuliwa kwa mabomu yaliyotegwa kwenye gari karibu na kambi ya jeshi la Sudan mjini Khartoum.
Wakati huohuo, Baraza la Usalama na Ulinzi la Sudan limelaani shambulizi hilo dhidi ya Waziri Mkuu Abdulla Hamdok na kukitaja kama kitendo haramu, kinachoonyesha hatari inayoikabili Sudan kutoka ndani na nje ya nchi.
Ripoti zinaeleza kuwa, Abdullah Hamdouk hakupata majeraha yoyote katika shambulio hilo la bomu ingawa mmoja wa walinzi wake amejeruhiwa katika tukio hilo. Inaelezwa kuwa, mlipuko huo ulitokea jirani na gereza la Kobar anamotumikia kifungo aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.
Abdulla Hamdok aliteuliwa kuchukua wadhifa wa Waziri Mkuu wa Sudan Agosti mwaka jana baada ya maandamano makubwa yaliyomuondoa madarakani Omar al-Bashir na kisha jeshi kuchukua utawala wa nchi, ambalo nalo lililazimika kukabidhi madaraka kwa utawala wa raia.