Washukiwa 44 wa Boko Haram wapatikana wameaga dunia gerezani Chad
(last modified Sun, 19 Apr 2020 03:39:31 GMT )
Apr 19, 2020 03:39 UTC
  • Washukiwa 44 wa Boko Haram wapatikana wameaga dunia gerezani Chad

Makumi ya washukiwa wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wameaga dunia katika mazingira ya kutatanisha gerezani nchini Chad.

Hayo yalitangazwa jana Jumamosi kwa njia ya televisheni na Youssouf Tom, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa serikali na kuongeza kuwa, yumkini wafungwa hao waliuawa au kujiua kwa sumu. Amesema wafungwa 44 walipatikana wameaga dunia gerezani siku ya Alkhamisi, na uchunguzi wa kimaabara uliofanywa unaonyesha kuwa walikufa kwa sumu kali iliyowasababishia mshtuko wa moyo. 

Hata hivyo, Mahamat Nour Ahmed Ibedou, Katibu Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Chadian Convention for the Protection of Human Rights (CTDDH) amedai kuwa wafungwa hao ni miongoni mwa washukiwa 58 wa Boko Haram ambao walikuwa wanazuiliwa chini ya mazingira magumu bila chakula wala maji katika gereza la N'Djamena.

Waziri wa Sheria, Djimet Arabi amekanusha madai hayo ya kuteswa wafungwa hao, akisisitiza kuwa mada za sumu zilipatikana kwenye matumbo yao na haijabainika iwapo walijiua au waliuawa.

Wanajeshi wa Chad

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Idriss Déby wa Chad kusema kuwa, wanajeshi wa nchi yake waliotumwa kupambana na magenge ya kigaidi katika eneo la Ziwa Chad na eneo zima la Sahel watarejea nyumbani na hawatoshiriki tena kwenye operesheni za kupambana na magenge hayo.

Majeshi ya Chad yalitangaza kumaliza opereseheni zao dhidi ya Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad huku serikali ya N'Djamena ikisema kuwa wanajeshi 52 wameuawa katika operesheni ya mwisho iliyoua pia maelfu ya magaidi.