Mali za viongozi wa zama za Omar al-Bashir nchini Sudan zataifishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60491-mali_za_viongozi_wa_zama_za_omar_al_bashir_nchini_sudan_zataifishwa
Serikali ya Sudan imetangaza kuwa, mali za viongozi wa zamani katika kipindi cha uongozi wa Omar Hassan al-Bashir Rais wa zamani wa nchi hiyo zimetaifishwa na kufanywa kuwa mali ya umma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2020 07:22 UTC
  • Mali za viongozi wa zama za Omar al-Bashir nchini Sudan zataifishwa

Serikali ya Sudan imetangaza kuwa, mali za viongozi wa zamani katika kipindi cha uongozi wa Omar Hassan al-Bashir Rais wa zamani wa nchi hiyo zimetaifishwa na kufanywa kuwa mali ya umma.

Muhammad al-Faki Suleiman afisa kijana zaidi katika Baraza la Utawala wa mpito nchini Sudan amesema kuwa, Kamati ya Kuvunja Serikali ya Omar al-Bashir imetaifisha mali nyingi za viongozi wa kipindi cha serikali ya al-Bashir na kuzifanya kuwa mali ya taifa.

Kadhalika afisa huyo wa Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan ameeleza kwamba, miongoni mwa mali hizo ni miliki mbalimbali pamoja na mamilioni ya dola.

Ripoti zinaeleza kuwa, miongoni mwa mali zilizokuwa zikimilikiwa na maafisa wa serikali ya zamani ya al-Bashir pamoja na familia zao ni Shirika la Usafiri na Uchukuzi la Nahri ambapo mali zake zinakadiriwa kufikia dola milioni 450.

Rais wa zamani wa Sudan Omar Hassan al-Bashir

Muhammad al-Faki Suleiman amebainisha kuwa, kundi dogo la asilimia 2 lililotawala nchini Sudan kwa miaka mingi lilikuwa likimiliki utajiri mkubwa na kuwaacha wananchi wa nchi hiyo katika umasikini mkubwa. 

Mwezi Januari mwaka huu pia, serikali ya Sudan ilitwaa mali za chama cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir kilichovunjwa na kupigwa marufuku nchini humo.

Omar Hassan al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo tarehe 11 Aprili mwaka jana kufuatia maandamano na malalamiko ya miezi kadhaa ya wananchi. Maandamano hayo yalichochewa na hali mbaya ya uchumi, ufisadi mkubwa na utumiaji mbaya wa madaraka wa al Bashir.