Libya: Watawala wa Imarati ndio wanaosababisha maafa nchini mwetu
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa ya Libya amesema kuwa, watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ndio wanaosababisha maafa nchini Libya kutokana na wanamgambo wake walioko chini ya jenerali muasi Khalifa Haftar kutumia gesi za sumu katika mashambulizi yao.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imemnukuu Fat'hi Bashagha akisema hayo kujibu uingiliaji wa Umoja wa Falme za Kiarabu katika masuala ya ndani ya Libya na uungaji mkono wa Imarati kwa jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza wanamgambo wa kundi linalojiita "Jeshi la Taifa la Libya" na kusisitiza kuwa Abu Dhabi ndiyo inayosababisha maafa yote yanayoendelea hivi sasa huko Libya.
Amesema, wanamgambo wa Khalifa Haftar wamekuwa wakitumia gesi za sumu katika mapigano yao na askari wa Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa katika eneo la Swalahuddin la kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli na kuua watu wengi kwa gesi hiyo ya sumu.
Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Maridhiano ya Kiataifa ya Libya ameitaka jamii ya kimataifa kutambua hasara kubwa inayosababishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa wananchi wa Libya.
Libya haijawahi kuwa na utulivu wa hata siku moja tangu zilizopoanza kampeni za kumpindua kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mwaka 2011. Nchi za Magharibi chini ya mwavuli wa NATO ziliivamia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu sambamba na kugawa silaha nyingi kwa makundi tofauti hasimu ambayo hadi leo hii yanaendelea kupigana yenyewe kwa yenyewe.
Hivi sasa kuna serikali mbili nchini Libya, moja ni ya mjini Tripoli ya Maridhiano ya Kimataifa ambayo inatamuliwa kimataifa na nyingine ni ya Tobrok, mashariki mwa Libya chini ya jenerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi.