Serikali ya Mpito Sudan: Jamaa wa al Bashir wanapanga njama ya mapinduzi
Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan ametangaza kuwa, watu wa karibu na rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir wanapanga njama ya mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amekituhumu chama kilichopigwa marufuku cha Kongresi ya Kitaifa kilichokuwa kikiongozwa na Omar al Bashir kuwa kinafanya mikakati ya kupenya katika safu za vikosi vya jeshi na kutayarisha mazingira ya kufanyika mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito.
Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan amesema kuwa, ushahidi unaonyesha kuwa, chama cha Kongresi ya Taifa kinavuruga kazi za serikali ya mpito na kuwavunja moyo wananchi kuhusiana na mapinduzi yaliyoiondoa madarakani serikali ya al Bashir, lakini taifa la Sudan litaendelea kuyanunga mkono na kuyalinda mapinduzi hayo.
Al Burhan ameongeza kuwa, kwa sasa vyombo vya sheria vya Sudan vinachunguza na kutathmini ripoti na taarifa zote zinazohusiana na jaribio la mapinduzi dhidi ya utawala wa sasa na kwamba mtu yeyote anayeshambulia mapinduzi anashambulia Sudan na atachukuliwa hatua.
Omar Hassan al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo tarehe 11 Aprili mwaka jana kufuatia maandamano na malalamiko ya miezi kadhaa ya wananchi. Maandamano hayo yalichochewa na hali mbaya ya uchumi, ufisadi mkubwa na utumiaji mbaya wa madaraka wa al Bashir.