WHO yatangaza mlipuko mpya wa ugonjwa wa Polio nchini Niger
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa Niger imekumbwa na mlipuko mpya wa ugonjwa wa kupooza viungo vya mwili wa Polio, baada ya kusimamishwa utoaji wa chanjo ya ugonjwa huo kufuatia mlipuko wa janga la Corona.
Pascal Mkanda, mratibu wa WHO wa kutokomeza Polio barani Afrika amesema watoto wawili wamethibitishwa kukumbwa na ugonjwa huo hatarishi na kwamba mmoja wao tayari amepooza viungo vyake vya mwili.
Amesema mlipuko wa sasa hauna uhusiano wowote na ule ambao Niger ilifanikiwa kuudhibiti mwaka jana, na kwamba iwapo kampeni ya utoaji chanjo itaendelea kusimamishwa huenda watoto wengi zaidi wakaambukizwa virusi vya ugonjwa huo na hata kupooza.
WHO ilitangaza mapema mwezi huu kuwa maafisa wake wameshurutishwa kusimamisha shughuli za kutoa chanjo ya Polio hadi Juni Mosi, ili jitihada zote zielekezwe katika mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 (Corona).
Hii ni katika hali ambayo, Mei mwaka jana Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa huenda likatangaza mapema mwaka huu kuwa bara Afrika halina tena ugonjwa wa kupooza wa Polio.
Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (CDC), ugonjwa huo wa kupooza wa Polio ambao aghalabu huwakumba watoto wenye umri wa miaka mitano umeshaua watu 1,469 kufikia Jumanne ya jana, huku kesi 33,500 zikirekodiwa.
Kesi ya mwisho ya ugonjwa wa Polio barani Afrika iliripotiwa nchini Nigeria Agosti mwaka 2016. Hata hivyo Aprili mwaka uliofuata wa 2017, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) yalizindua kampeni ya chanjo ya aina yake kuwahi kufanyika katika bara la Afrika dhidi ya Polio, iliyolenga watoto milioni 116 katika nchi 13 za Afrika Magharibi na Kati.