HRW: Shambulizi la 'drone' ya Imarati liliua raia 8 Tripoli, Libya
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli mwishoni mwa mwaka jana liliua na kujeruhi raia wasio na hatia.
Katika ripoti yake ya jana Jumatano, HRW imesema shambulizi hilo la anga la Novemba 18 mwaka jana 2019 lililenga kiwanda cha biskuti jijini Tripoli, ambapo raia 8 waliuawa huku wengine 27 wakijeruhiwa.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeeleza bayana kuwa, inaonekana kuwa UAE haijachukua hatua za kupunguza mauaji ya raia katika mashambulizi yake. HRW imezitaka mamlaka husika za Abu Dhabi kuanzisha uchunguzi huru wa tukio hilo la Novemba 18.
Agosti mwaka jana pia, Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri MKuu Fayez al-Sarraj ilitangaza kuwa, ndege zisizo na rubani (drone) za Imarati zimedondosha mabomu kusini mwa Tripoli na kupelekea raia watatu kuuawa.
Haya yanajiri wiki moja baada ya Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa ya Libya kusema kuwa, watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu ndio wanaosababisha maafa nchini Libya kutokana na wanamgambo wake walioko chini ya jenerali muasi Khalifa Haftar kutumia gesi za sumu katika mashambulizi yao.
Serikali hiyo inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imeitaka jamii ya kimataifa kutambua hasara kubwa inayosababishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa wananchi wa Libya.