Tunisia yaisaidia Uturuki kufikisha misaada Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60860-tunisia_yaisaidia_uturuki_kufikisha_misaada_libya
Serikali ya Tunisia imeiruhusu ndege ya Uturuki ambayo inasemekana ilikuwa na misaada ya kitiba kwa ajili ya Libyan itue nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2020 19:30 UTC
  • Tunisia yaisaidia Uturuki kufikisha misaada Libya

Serikali ya Tunisia imeiruhusu ndege ya Uturuki ambayo inasemekana ilikuwa na misaada ya kitiba kwa ajili ya Libyan itue nchini humo.

Ofisi ya Rais wa Tunisia imetangaza Ijumaa kuwa, ndege ya Uturuki iliyokuwa imesheheni misaada ya kitiba imeruhusiwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Djerba–Zarzis  kusini mwa Tunisia na kwamba wakuu wa Tunisia watafikisha shehena hiyo nchini Libya.

Serikali ya Tunisia imesisitiza kuwa,  hakuna jeshi lolote la kigeni litakaloruhusiwa kutumia ardhi ya Tunisia kuingilia kijeshi Libya. Taarifa ya Ofisi ya Rais wa Tunisia imebainiwa kuwa: "Maafisa wa usalama na forodha wa Tunisia wataifikisha misaada katika eneo la mpaka la Ras Ajdir na itakabidhiwa kwa wakuu wa Libya."

Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya (GNU), yenye makao yake Tripoli, inapata uungaji mkono wa kijeshi wa Uturuki na ndiyo iliyotumiwa misaada hiyo ya kitiba.

Afisa mmoja wa Tunisia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, ndege hiyo ya misaada ya Uturuki haingeweza kutua katika viwanja vya ndege vya Libya kutokana na ukosefu wa usalama. Tunisia imesisitiza kuwa kutua ndege hiyo ya Uturuki nchini humo kusitathminiwe kwa nia nyingine isipokuwa tu katika fremu ya msaada wa kibinadamu.

Aprili mwaka jana, jenarali muasi Khalifa Haftar alianzisha mapigano kwa lengo kuukalia kwa mabavu mji wa Tripoli na kuitimua serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj na inayotambuliwa kimataifa.

Baadhi ya duru za habari zimewanukulu wafuasi wa Haftar wakidai kuwa, Uturuki ina kituo cha siri cha kijeshi nchini Tunisia ambacho kinatumiwa kutekeleza oparesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Haftar. Tunisia imekanusha madai hayo.

Hivi karibuni,  Rais Kais Saied wa Tunisia alitangaza kuwa nchi yake inapinga njama za kuigawa Libya vipande vipande. Aidha alisisitiza kuwa Tunisia lazima ihusishwe na utatuzi wa mgogoro wa Libya.