Watu 26 wauawa katika mapigano ya kikabila kusini mwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60976-watu_26_wauawa_katika_mapigano_ya_kikabila_kusini_mwa_sudan
Watu wasiopungua 26 wanaripotiwa kuuawa kusini mwa Sudan na wengine 19 kujeruhiwa baada ya kuibuka mapigano ya kikabila katika jimbo la Kordofan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2020 06:34 UTC
  • Watu 26 wauawa katika mapigano ya kikabila kusini mwa Sudan

Watu wasiopungua 26 wanaripotiwa kuuawa kusini mwa Sudan na wengine 19 kujeruhiwa baada ya kuibuka mapigano ya kikabila katika jimbo la Kordofan Kusini.

Naibu Mkuu wa Majeshi ya Sudan Abdallah al-Bashir amethibitisha kutokea mapigano hayo na kueleza kwamba, watu 26 wameuawa katika mapigano hayo ya siku mbili yaliyojiri katika mji wa Kadugli.

Duru rasmi zinasema kuwa, machafuko hayo ambayo ni ya tatu kuibuka katika tangu kuanza mwezi huu wa Mei, ni changamoto kubwa kwa Serikali ya Mpito ya nchi hiyo.

Serikali ya Mpito ya Sudan imetangaza kuwa, tayari imeanzisha uchunguzi kuhusiana na mapigano hayo.

Wiki iliyopita, kwa akali watu 30 waliuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mapigano ya kikabila baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu katika mkoa wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan

Aidha mapema mwaka huu, watu 36 waliuawa katika mapigano mengine ya kikabila baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu katika mkoa huo wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Umwagaji damu unaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Sudan likiwemo eneo la Darfur, licha ya serikali mpya ya Sudan kuahidi kumaliza migogoro nchini humo ukiwemo ule wa Darfur ambao umepelekea watu wasiopungua laki tatu kuuawa na wengine milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi.

Tangu mwezi Disemba 2018, Sudan ilikumbwa na maandamano makubwa ya wananchi waliolalamikia utendaji mbovu wa serikali ya Omar al-Bashir. Maandamano hayo yaliendelea hadi mwezi Aprili 2019 wakati jeshi lilipoingilia kati na kumuondoa kwa nguvu madarakani Omar al Bashir. Baada ya hapo ilifuatia miezi kadhaa ya maandamano ya wananchi hadi jeshi lilipolazimika kuunda serikali ya mpito na kuvunja Baraza la Kijeshi lililoundwa baada ya kupinduliwa al Bashir.