Serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya yataka kukatwa uhusiano na Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61015-serikali_ya_mwafaka_wa_kitaifa_ya_libya_yataka_kukatwa_uhusiano_na_imarati
Mjumbe wa Baraza la Rais la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya, sambamba na kuashiria ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na uungaji mkono wa Imarati kwa jenerali muasi Khalifa Haftar, ametaka kukatwa uhusiano wa Tripoli na Abu Dhabi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 16, 2020 06:32 UTC
  • Serikali ya mwafaka wa kitaifa ya Libya yataka kukatwa uhusiano na Imarati

Mjumbe wa Baraza la Rais la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya, sambamba na kuashiria ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na uungaji mkono wa Imarati kwa jenerali muasi Khalifa Haftar, ametaka kukatwa uhusiano wa Tripoli na Abu Dhabi.

Mohammad Amari Zayed, Mjumbe wa Baraza la Rais la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ametoa matamshi hayo katika radiamali yake kwa ripoti hiyo ya siri ya Umoja wa Mataifa ambapo amelitaka baraza hilo pamoja na Fayez al-Sarraj, Rais wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa kuitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kukata uhusiano na Imarati. Katika barua aliyomwandikia Al-Sarraj Zayed amesema kuwa Libya ni lazima iitangaze Imarati kuwa nchi vamizi na kwamba kuendelea kunyamazia kimya jinai zisizohalalishika za nchi hiyo, kutasababisha umwagikaji zaidi wa damu ya raia wa Libya. 

Mtawala wa Imarati

Mohammad Amari Zayed ameongeza kwamba baraza hilo ni lazima litekeleze majukumu yake katika kuzuia kumwagika damu zaidi ya Walibya sambamba na kutoa amri kwa wizara zote, asasi za serikali, balozi na jumbe za kidiplomasia nje ya nchi kuiburuza Imarati katika mahkama za kimataifa. Mjumbe wa Baraza la Rais la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya pia ametaka kuamiliana na serikali ya Abu Dhabi kama adui.