Magaidi 21 waliopanga kuvuruga sherehe za Iddi wauawa Sinai, Misri
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza habari ya kuuawa wanachama 21 wa genge moja la kigaidi katika operesheni mbili tofauti zilizofanyika katika Peninsula ya Sinai.
Taarifa ya jana Jumamosi ya wizara hiyo imesema, magaidi hao wameangamizwa katika operesheni mbili za jeshi la Misri katika mkoa wa Sinai Kaskazini, wakijiandaa kufanya wimbi la mashambulizi ya kigaidi wakati huu wa sherehe za Iddul-Fitr.
Waislamu wa Misri wamejiunga na wenzao kote duniani hii leo katika maadhimisho ya sikukuu ya Iddul-Fitr, inayoashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imeongeza kuwa, maafisa wawili wa serikali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wamejeruhiwa kwenye operesheni hizo dhidi ya maficho ya magaidi.

Kadhalika jeshi la Misri limefanikiwa kukamata silaha za aina mbalimbali zilizokuwa mikononi mwa magaidi hao.
Mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mapigano baina ya maafisa usalama na magenge ya kigaidi ambayo yameshadidisha mashambulizi yake katika miaka ya hivi karibuni, hususan baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mohammad Morsi hapo mwaka 2013.