Algeria: Tutaendelea na upatanishi hadi kutatuliwa mzozo wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61360-algeria_tutaendelea_na_upatanishi_hadi_kutatuliwa_mzozo_wa_libya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa, nchi yake itaendeleza juhudi za kupunguza mizozo na kuzikinaisha pande nyingine nchini Libya ili zishiriki mazungumzo ya kisiasa ya kutatua mzozo wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 02, 2020 03:00 UTC
  • Algeria: Tutaendelea na upatanishi hadi kutatuliwa mzozo wa Libya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa, nchi yake itaendeleza juhudi za kupunguza mizozo na kuzikinaisha pande nyingine nchini Libya ili zishiriki mazungumzo ya kisiasa ya kutatua mzozo wa nchi hiyo.

Sabri Boukadoum aliyasema hayo jana Jumatatu katika kikao cha bunge kilichoandaliwa kwa ajili ya kujadili msimamo wa Algeria kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa na hali ya jamii za wachache nje ya nchi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema: "Tunafanya juhudi za kupunguza mizozo nchini Libya kwa kuzishirikisha na kuzikinaisha pande husika zikumbatie mwenendo wa kisiasa  wenye malengo ya amani."

Sabri Boukadoum, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria

Katika wiki kadhaa zilizopita, Algeria ilianzisha juhudi za kidiplomasia kwa lengo la kutatua mgogoro wa Libya kama ambavyo imetoa pendekezo la kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya pande kadhaa za mgogoro wa Libya hapo mwezi Julai. Hivi karibuni Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Algeria alinukuliwa akisema kuwa, nchi yake ilikuwa karibu kutatua mzozo wa Libya na kuanzisha mwenendo wa kisiasa nchini humo, ingawa juhudi hizo hazikufikia natija ya kuridhisha.