Tuhuma mpya dhidi ya Omar al Bashir zaanza kufuatiliwa nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61530-tuhuma_mpya_dhidi_ya_omar_al_bashir_zaanza_kufuatiliwa_nchini_sudan
Mkuu wa Kamati ya Kupambana na Ufisadi ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Uongozi la Sudan ametangaza habari ya kuanza kufuatiliwa tuhuma mpya zinazomkabilia rais wa zamani wa nchi hiyo, Jenerali Omar Hassan Ahmad al Bashir.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 10, 2020 21:56 UTC
  • Tuhuma mpya dhidi ya Omar al Bashir zaanza kufuatiliwa nchini Sudan

Mkuu wa Kamati ya Kupambana na Ufisadi ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Uongozi la Sudan ametangaza habari ya kuanza kufuatiliwa tuhuma mpya zinazomkabilia rais wa zamani wa nchi hiyo, Jenerali Omar Hassan Ahmad al Bashir.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Mohamed al Faki Suleiman amesema, kamati yake imeanza kufanya uchunguzi mpya kuhusu tuhuma nyingine za Omar al Bashir nazo ni za kufuja na kutumia vibaya mali ya serikali na ya umma kwa manufaa yake binafsi.

Ameongeza kuwa, uchunguzi wa kamati yake umegundua kuwa, kila mwezi zilikuwa zinaingizwa dola milioni 20 katika hesabu maalumu ya Omar al Bashir nje ya utaratibu wa kisheria.

Kamati ya Kupambana na Ufisadi nchini Sudan imeifunga hesabu maalumu ya benki ya al Bashir pamoja na maduka matano ya kubadilisha fedha kwa madai ya kutumika kuudhaminia fedha utawala wa Jenerali Omar al Bashir.

Maandamano yaliyomng'oa madarakani al Bashir nchini Sudan

 

Kwa upande wake, Mohamed al Hassan al Amin, wakili wa al Bashir amesema hana taarifa zozote kuhusu kuweko hesabu kama hiyo na miamala kama hiyo ya Benki na ametaka rais huyo wa zamani wa Sudan afanyiwe uadilifu wa kisiasa.

Mwezi Disemba 2018 Sudan ilianza kukumbwa na maandamano ya nchi nzima ya kupinga serikali ya Jenerali Omar al Bashir. Maandamano hayo yaliendelea hadi mwezi Aprili 2019 wakati wanajeshi walipofanya mapinduzi ya kumng'oa madarakani al Bashir na kudhibiti uongozi. Suala hilo liliwakasirisha wananchi walioendelea na maandamano hayo hadi jeshi lilipolazimika kukubali kuunda Baraza la Uongozi la kushirikisha matabaka mbalimbali. Hadi hivi sasa makumi ya viongozi wa serikali ya al Bashir wameshatiwa mbaroni kwa tuhuma za jinai, ufisadi na masuala ya kisiasa.