17 wauawa na kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu Tripoli, Libya
(last modified Thu, 11 Jun 2020 07:57:08 GMT )
Jun 11, 2020 07:57 UTC
  • 17 wauawa na kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu Tripoli, Libya

Kwa akali watu saba wameuawa na wengine zaidi ya kumi wamejeruhiwa katika mlipuko wa bomu uliotokea karibu na mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mlipuko huo umesababishwa na mabomu ya kutegwa ardhini ya vikosi vya  jenerali muasi Khalifa Haftar.

Habari zaidi zinasema kuwa, miongoni mwa waliopoteza maisha katika mlipuko huo ni mwanamke mmoja na afisa polisi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Mashuhuda wanasema milipuko mitatu mikubwa ilisikika wakati wa tukio hilo.

Katika hatua nyingine, makumi ya makaburi ya umati yamegunduliwa katika mji wa Tarhauna uliokuwa mikononi mwa wapiganaji wa Haftar, umbali wa kilomita 90 kusini mwa Tripoli.

Haftar ambaye vikosi vyake vinaelekea kushindwa kikamilifu Libya

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Fathi Bashagha, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya nchi hiyo ambaye amebainisha kuwa, "tumegundua jinai za kutisha zilizofanywa na wanamgambo waliokuwa wakishikilia Tarhauna. Tumepata makaburi ya umati ambapo baadhi yazo yana makumi ya maiti. Aidha tumegundua shehena zilizokuwa na watu waliouawa kwa kuteketezwa moto wakiwa hai." 

Wapiganaji wanaojiita jeshi la kitaifa la Libya chini ya Khalifa Haftar walianzisha mashambulizi makali mwezi Aprili 2019 kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji wa Tripoli. Hata hivyo muqawama wa wapiganaji wanaoiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa, umewafanya wapiganaji wa Haftar kupoteza udhibiti wa mji mkuu huo wa Libya, Tripoli na mji wa Tarhauna, ngome muhimu ya wanamgambo hao.