Kaburi la umati la kipindi cha utawala wa al Bashir lagunduliwa Sudan
Mwendesha mashtaka ya umma wa Sudan amesema kuwa kumegunduliwa kaburi la umati la kipindi cha utawala wa Omar al Bashir huko mashariki mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.
Taj Al-Sir Ali Al-Hebr amesema kuwa, uchunguzi kuhusiana na kadhia hiyo umekwishaanza. Ameongeza kuwa, baadhi ya washukiwa wa jinai hiyo na watu waliokuwa karibu na utawala wa Rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir wametoweka.
Afisa mmoja wa timu ya uchunguzi amesema kuwa, maiti za makumi ya watu zimepatikana katika kaburi hilo la umati lililoko mashariki mwa Khartoum.
Inasemekana kuwa, kaburi hilo la umati ni la wanachuo waliouawa mwaka 1998 wakati wanajaribu kutoroka kambi ya mafunzo ya huduma za jeshi. Vijana hao walimiminiwa risasi wakati walipokuwa wakitoroka kambi hiyo ya mafunzo wakiogopa kutumwa vitani huko Sudan Kusini kwa ajili ya kukabiliana na waasi wa Jeshi la Taifa la Ukombozi wa Watu Sudan (SPLA) wakati wa vita vya ndani nchini humo.
Rais Omar al Bashir aliondolewa madarakani mwaka 2018 kutokana na vuguvugu kubwa la wananchi waliokuwa wakipinga ufisadi uliokuwa umekita mizizi katika serikali yake na vilevile hali mbaya ya kiuchumi.