Waziri Mkuu wa Libya aonana na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61727-waziri_mkuu_wa_libya_aonana_na_rais_abdelmadjid_tebboune_wa_algeria
Waziri Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya Fayez al Sarraj ameonana na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria na pande mbili zimejadiliana njia za upatanishi na jinsi ya kutatua mgogoro wa Libya.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 20, 2020 23:14 UTC
  • Waziri Mkuu wa Libya aonana na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria

Waziri Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya Fayez al Sarraj ameonana na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria na pande mbili zimejadiliana njia za upatanishi na jinsi ya kutatua mgogoro wa Libya.

Shirika la habari la AFP limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, hiyo ni katika sehemu ya juhudi za Algeria za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa miaka mingi wa Libya.

Ikumbukwe kuwa tarehe 19 mwezi huu wa Juni, msemaji wa Ikulu ya Algeria, Belaid Mohand Usaid alisema kuwa, Algiers ina nia ya kuitisha mkutano utakaozishirikisha pande mbalimbali za Libya kama sehemu ya juhudi zake za kuyapatanisha makundi hayo.

Mpaka wa Algeria na Libya

 

Tangu mwaka 2015 mgogoro wa Libya umegeuka kuwa uwanja wa ushindani wa madola mbalimbali ajinabi. Baadhi ya madola hayo yanaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa iliyoundwa kwa usimamiaji wa Umoja wa Mataifa na wengine wanamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya."

Tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka jana 2019, kundi la Khalifa Haftar lilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa tamaa ya kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

Algeria nayo imetangaza kuwa, kwa vile ina mpaka mrefu na Libya unaokadiriwa kufikia kilomita elfu moja, ni jukumu lake kuzipatanisha pande hasimu za Libya na kupinga uingiliaji wowote wa madola ya kigeni, kwani matukio ya Libya yanaiathiri moja kwa moja Algeria.