May 01, 2016 14:09 UTC
  • Askari 15 wa Somalia wauawa katika hujuma ya al-Shabaab

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limeua askari 15 wa jeshi la Somalia sanjari na kuchukua udhibiti wa mji wa Runirgood, yapata kilomita 180 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.

Kapten Nur Ali, afisa mwandamizi wa jeshi la Somalia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanamgambo wa al-Shabaab wamevamia kambi ya jeshi katika mji huo kwa kutumia gari lililokuwa na bomu kabla ya kujiri ufyatulianaji risasi kwa muda. Ameongeza kuwa, kambi hiyo ilikuwa na wanajeshi wachache wa Kisomali na kwamba hakukuwa na askari yeyote wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja Afrika AMISOM, ndiposa wakazidiwa nguvu na magaidi hao. Hata hivyo amesema kuwa wamefanikiwa kuangamiza wanachama 10 wa al-Shabaab.

Hii ni katika hali ambayo, kundi hilo la kigaidi na kitakfiri limedai kuwa limeua makumi ya wanajeshi wa Somalia katika hujuma hiyo.

Abaluaziz Abu Musab, msemaji wa al-Shabaab katika maswala ya kijeshi amenukuliwa na Reuters akidai kuwa, wameua askari 32 wa Somalia na kuteka magari matatu ya kijeshi mbali na kuchukua udhibiti wa mji wa Runirgood.

Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMISOM, waliwasili nchini Somalia mwaka 2007 kwa lengo la kurejesha usalama ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Tags