Watu wa Sudan waandamana wakitaka mabadiliko ya haraka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61926-watu_wa_sudan_waandamana_wakitaka_mabadiliko_ya_haraka
Wananchi wa Sudan wameandamana katika mji mkuu, Khartoum na miji mingine ya nchi hiyo wakitaka mabadiliko ya haraka na haki kwa waliouawa katika maandamano ya mwaka jana yalyopelekea jeshi kumuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 30, 2020 22:00 UTC
  • Watu wa Sudan waandamana wakitaka mabadiliko ya haraka

Wananchi wa Sudan wameandamana katika mji mkuu, Khartoum na miji mingine ya nchi hiyo wakitaka mabadiliko ya haraka na haki kwa waliouawa katika maandamano ya mwaka jana yalyopelekea jeshi kumuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir.

Taarifa zinasema polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika barabara ya kuelekea katika uwanja wa ndege wa Khartoum.

Maandamano hayo yameitishwa na Jumuiya ya Wataalamu wa Sudan na 'Kamati za Mapambano'. Makundi hayo mawili yalikuwa na nafasi kubwa katika maandamano yaliyomuondoa Al Bashir madarakani.

Waandamanaji walisikika wakitoa nara maarufu ya 'Uhuru, Amani na Uadilifu', ambayo ilitumiwa katika harakati ya kumuondoa madarakani Al Bashir.

Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok amejaribu kuwatuliza waandamanji kwa kusema matakwa yao ni halali ni yanatakikana ili kurekebisha mkondo wa mapinduzi.

Amesema  muungano wa kiraia na kijeshi unaotawala Sudan hivi sasa katika kipindi cha mpito uunatilia maanani matakwa ya wananchi. Hatahivyo amesema kuna matatizo mengi ambayo yanatishia utawala wa mpito nchini humo.

Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok

Aidha amesema katika siku chache zijazo kutachukuliwa maamuzi muhimu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii huku akitahadharisha kuwa baadhi watajaribu kutumia maamuzi hayo kuchochea ghasia. Taarifa zinasema watu watiifu kwa Al Bashir nao pia wanapanga maandamano.

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka 2018 dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka 2019 lilimuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir. Hatimaye baada ya vuta nikuvute hatimaye nchini Sudan kuliundwa serikali ya mpito itakayoongoza kwa kipindi cha miaka mitatu kuelekea uchaguzi mkuu.