Waasi wa SPLM nchini Sudan watangaza kusitisha vita kwa miezi saba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61961-waasi_wa_splm_nchini_sudan_watangaza_kusitisha_vita_kwa_miezi_saba
Tawi la kaskazini la kundi la waasi la SPLM la Sudan limetangaza kuongeza muda wa kusitisha vita kwa miezi mingine saba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2020 07:56 UTC
  • Waasi wa SPLM nchini Sudan watangaza kusitisha vita kwa miezi saba

Tawi la kaskazini la kundi la waasi la SPLM la Sudan limetangaza kuongeza muda wa kusitisha vita kwa miezi mingine saba.

Mkuu wa kundi hilo Bw. Abdel-Aziz Al-Hilu amesema, watasimamisha vita katika maeneo yote wanayoyadhibiti kuanzia tarehe 1 Julai mpaka mwishoni mwa mwezi wa Januari mwakani, na amewataka wapiganaji wa kundi hilo kufuata taarifa hiyo isipokuwa wakati wa kujilinda au kulinda usalama wa raia.

Amesema, kitendo hicho ni kwa ajili ya kutatua suala la Sudan kwa njia ya amani na kutoa mchango kwa mafanikio ya mazungumzo ya amani yanayoendelea sasa.

Tawi la kaskazini la kundi la waasi la SPLM limekuwa likipambana na serikali katika eneo la Kordofan Kusini na pia eneo la Blue Nile.

Mazungumzo ya amani baina ya serikali ya Sudan na makunid ya waasi katika maeneo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile yamekuwa yakifanyika, Juba, Sudan kusini kuanzia Oktoba mwaka jana.

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan Abdallah Hamdok

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan Abdallah Hamdok amesema kupatikana amani ya kudumu ni kipaumbele cha serikali anayoiongoza. Mazungumzo ya Juba yametajwa kuwa hatua ya kwanza katika mazungumzo ambayo yanapaswa kufikia amani kamili ya kudumu nchini Sudan.