Mawaziri wanne muhimu wa serikali ya mpito Sudan wapigwa kalamu nyekundu
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amewabadilisha mawaziri wanne na maafisa wengine waandamizi watatu wanaoongoza wizara za serikali ikiwa ni sehemu ya mabadiliko makubwa aliyotangaza kuyafanya katika baraza la mawaziri la serikali hiyo ya mpito anayoiongoza.
Taarifa iliyotolewa na serikali imesema, mawaziri wanne waliobadilishwa ni wa fedha, mambo ya nje, nishati na afya.
Ijapokuwa duru za serikali zilikuwa zimetangaza awali kwamba baraza la mawaziri linaloongozwa na Hamdok litafanyiwa mabadiliko, lakini wengi hawakutegemea kama miongoni watakoondoka serikalini ni pamoja na waziri wa fedha Ibrahim al-Badawi, ambaye ameongoza jitihada za kuleta uthabiti katika uchumi wa nchi hiyo uliokuwa katika hali mbaya pamoja na kujenga mashirikiano na wafadhili wa kigeni.
Taarifa ya serikali ya Khartoum imefafanua kuwa Waziri Mkuu Abdallah Hamdok amemfuta kazi waziri wa afya Akram Ali Altom na amekubali kujiuzulu kwa al-Badawi na mawaziri wengine. Hamdok ameteua maafisa wengine wapya saba kuongoza nafasi za wizara hizo zilizoachwa wazi.
Abdalla Hamdok anaongoza serikali ya mateknokrati chini ya makubaliano ya kugawana madaraka kati ya jeshi na makundi ya kiraia ili kuongoza serikali ya mpito kwa kipindi cha miezi 39 kufuatia kuondolewa madarakani rais wa muda wa mrefu wa nchi hiyo Omar al-Bashir Aprili 2019.
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, Heba Ahmed Ali, afisa mwandamizi katika wizara ya fedha ndiye atakayeshikilia kwa muda wadhifa wa kuongoza wizara hiyo.
Mabadiliko ya bazara la mawaziri la Sudan yamejiri siku tisa baada ya maandamano makubwa ya malalamiko ya wananchi waliowataka viongozi wa serikali ya mpito wafanye mageuzi ya kasi na mapana zaidi.
Wakati maandamano hayo yakiendelea, Waziri Mkuu Hamdok aliahidi kuchukua maamuzi kadhaa makubwa bila kutoa ufafanuzi. Mapema wiki hii, kiongozi huyo wa kiraia aliwafuta kazi mkuu wa jeshi la polisi na naibu wake ambao walikuwa wakionekana na makundi ya kutetea demokrasia nchini Sudan kama watu wenye mfungamano na utawala uliong'olewa wa al-Bashar.../