Mahakama ya ICC yaanza kufuatilia faili la makaburi ya umati huko Libya
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake huko Hague Uholanzi imeanza kufuatilia uwepo wa makaburi ya umati katika mji wa Tarhuna huko Libya.
Ujumbe kutoka mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai umekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Ofisi ya Uchunguzi ya Mwendesha Mashtaka wa Libya ili kuchunguza kadhia hiyo ya kuwepo makaburi ya umati na maeneo yaliyotegwa mabomu ardhini katika mji wa Tarhuna nchini Libya.
Ujumbe huo tajwa wa ICC sambamba na kupata taarifa kuhusu uwepo wa makaburi hayo ya umati na mabomu ya kutegwa ardhini, umetaka kushtakiwa wale wote waliohusika katika kesi mbili hizo. Makaburi ya umati yamegunduliwa katika mji wa Tarhuna baada ya wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya wanaoongozwa na Jenerali Muasi Khalifa Haftar kuondoka katika mji huo.
Kundi hilo linalojiita jeshi la kitaifa la Libya ambalo limekuwa likidhibiti maeneo ya mashariki mwa Libya kwa miaka kadhaa sasa kutokana na uungaji mkono wa Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi; liliushambuliaanza kutekeleza mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa Libya Tripoli tangu Aprili mwaka jana hata hivyo limeshindwa kuuteka mji mkuu huo.