Waziri Mkuu mpya ateuliwa nchini Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62437-waziri_mkuu_mpya_ateuliwa_nchini_tunisia
Kufuatia kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia baada ya kujiuzulu Waziri Mkuu Elyes Fakhfakh, rais wa nchi hiyo Kais Saied, amemteua waziri wa mambo ya ndani Hichem Mechichi kuwa waziri mkuu mpya na kumtaka aunde baraza jipya la mawaziri.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 27, 2020 01:29 UTC
  • Waziri Mkuu mpya ateuliwa nchini Tunisia

Kufuatia kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia baada ya kujiuzulu Waziri Mkuu Elyes Fakhfakh, rais wa nchi hiyo Kais Saied, amemteua waziri wa mambo ya ndani Hichem Mechichi kuwa waziri mkuu mpya na kumtaka aunde baraza jipya la mawaziri.

Mechichi ni waziri mkuu wa nne Tunisia baada ya matukio ya kisiasa ya mwaka 2011 ambayo yalipelekea kupinduliwa dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali. Baada ya kuteuliwa, Mechichi ana muda wa siku 30 kuunda baraza jipya la mawaziri  na kisha kuwasilisha majina ya mawaziri hao bungeni ili wapigiwe kura. Kama hilo halitawezekana, basi Rais Kais Saied hatakuwa na budi ila kuvunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema.

Kuhusiana na nukta hiyo, Rais wa Tunisia amesema: "Kuwajibika kuhusu matakwa ya kisheria ya taifa na watu wasiojiweza ni kipaumbele chetu."

Elyes Fakhfakh alijiuzulu kama waziri mkuu wa Tunisia mnamo 15 Julai baada ya malalamiko ya baadhi ya vyama vya kisiasa, kikiwemo chama cha  Ennahda, kutokana na utendaji kazi wake dhaifu katika utatuzi wa mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo na pia kutokana na tuhuma za ufisadi dhidi yake. 

Spika wa Bunge la Tunisia Rachid al-Ghannouchi

Baada ya kupita miaka tisa ya matukio mengi ya kisiasa nchini Tunisia, nchi hiyo ingali inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na ufisadi. Aidha katika miezi ya hivi kariuni kulishuhudiwa malumbano ya kisiasa kati ya vyama mbali mbali vya kisiasa nchini Tunisia hasa baina ya Elyes Fakhfakh na Spika wa Bunge Rachid al-Ghannouchi na hivyo baadhi ya wataalamu wanasema kujiuzuli Fakhfakh kama waziri mkuu kulitokana na hitilafu baina yake na spika wa bunge.

Elyes Fakhfakh aliwahi kutangaza kuwa anahitilafiana sana na Rachid al-Ghannouchi ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Ennahda.

Hivi sasa wakati ambao Mechichi anapaswa kuunda baraza lake la mawaziri, kuna mpango uliowasilishwa wa kumuuzulu al-Ghannouchi kama spika wa bunge.

Hivi karibuni mirengo minne ya Bunge la Tunisia ambayo ni mrengo wa demokrasia, mrengo wa marekebisho ya kitaifa, mrengo  wa 'Tahiya Tunis' na mrengo wa kitaifa, yote imetangaza kuwa, imefikia muafaka kuhusu kutokuwa na imani na al-Ghannouchi. Kwa upande wake al-Ghannoouchi anasema mpango wa kutaka kulivunja bunge la Tunisia na kupiga kura ya kutokuwa na imani naye ni kinyume cha katiba.

Hichem Mechichi ambaye ni mkuu wa mrengo wa demokrasia katika bunge la Tunisia amesema:" Rachid al-Ghannouchi, kiongozi wa chama cha Ennahda ambaye ni spika wa bunge ana jukumu kubwa la kusimamia bunge lakini uongozi wke ni mbovu."

Mazingira ya kisiasa nchini Tunisia ni magumu sana; kusambaratika serikali ya Fakhfakh katika muda usiozidi miezi mitano baada ya kundwa ni jambo ambalo litashadidisha  matatizo ya nchi hiyo hasa wakati huu wa janga la corona.  Watunisia walitaraji serikali mpya ingeweza kutekeleza marekebisho ya haraka ya kiuchumi lakini hilo sasa limeakhirishwa. Aidha Tunisia inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiusalama kutokana na kupakana na Libya ambayo inakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu Tunisia Elyes Fakhfakh

Majina ya mawaziri yatawasilishwa katika bunge la Tunisia mapema mwezi Septemba kwa ajili ya kupigiwa kura na baraza hilo la mawaziri linapaswa kupata kura 109 kati ya 217 bungeni. Kwa kuzingatia hitilafu kubwa zilizopo baina ya Wabunge itakuwa vigumu sana kwa bunge kupiga kura ya kuwa na imani na baraza hilo la mwaziri la Mechichi.

Iwapo serikali ya Mechichi haitapata kura za wabunge kama inavyotakiwa kisheria, katiba ya nchi hiyo inampa rais uwezo wa kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema. Hatua kama hii itapelekea mgogogoro wa kisiasa wa nchi hiyo kuwa mbaya zaidi na hivyo kuzidisha matatizo ya kijamii na kiuchumi katika taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.