Tunisia yaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62502-tunisia_yaiunga_mkono_serikali_ya_mwafaka_wa_kitaifa_nchini_libya
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tunisia imetangaza kuwa, nchi hiyo itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 30, 2020 03:18 UTC
  • Tunisia yaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tunisia imetangaza kuwa, nchi hiyo itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya.

Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tunisia ilisema kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Salma Neifer amefanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya akisisitiza udharura wa kuendelea kuungwa mkono Serikali ya Tripoli inayoongozwa na Fayes al Sarraj.

Salma Neifer amesema Tunisia inafanya jitihada za kupatikana utatuzi wa kisiasa nchini Libya na kuwepo uthabiti wa kiuchumi na kijamii nchini humo.

Pande hizo mbili aidha zimetilia mkazo suala la kudumishwa mawasiliano na ushirikiano kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa mgogoro wa Libya.

Libya ilitumbukia katika mapigano na mgogoro wa kisiasa mwaka 2011 baada ya Marekani na nchi wanachama katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuparamia malalamiko ya wananchi na kumuondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.

Kwa sasa nchi hiyo ina serikali mbili; moja ikiwa ile inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa yenye makao makuu huko Tripoli, mji mkuu wa Libya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj, na serikali yenye makao makuu katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi inayosaidiwa na Imarati, Misri, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ulaya.