Ethiopia yalalamikia utendaji wa Marekani kuhusu mazungumzo ya Bwawa la al-Nahdha
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia imetangaza kuwa, mashinikizo ya Marekani dhidi ya nchi hiyo ili ifanye mazungumzo na Misri na Sudan kuhusiana na Bwawa la al-Nahdha yatakuwa na taathira hasi kwa uhusiano wa Washington na Addis Ababa.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia imeeleza kuwa, mashinikizo hayo kadhalika yatadhuru mwenendo wa mazungumzo ya nchi hiyo, Sudan na Misri kuhusiana na mvutano wa Bwawa la al-Nahdha.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia imesisitiza pia kuwa, juhudi za Marekani na Benki ya Dunia za kuishinikiza Addis Ababa ili itie saini makubaliano yasiyo na uwiano hazitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kutoa pigo kwa mazungumzo ya pande tatu kuhusu Bwawa la al-Nahdha.
Ethiopia imesisitiza kuwa, hakuna mashinikizo yoyote yale ambayo yataizuia nchi hiyo na kuifanya iachane na ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha na kwamba, katu azma ya nchi hiyo ya kukamilisha mradi huo haitatereka.
Wakati huo huo, balozi Dina Mufti, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia ametahadharisha kwamba, mashinikizo ya Marekani dhidi ya Ethiopia kuhusiana na kadhia ya Bwawa la al-Nahdha yatakuwa na taathira mbaya kwa uhusiano wa nchi mbili hizo.
Hivi karibuni Misri ilitangaza kusitisha mazungumzo yake na Ethiopia kuhusiana na kadhia ya bwawa hilo kutokana na kile ilichokieleza kuwa, hatua ya upande mmoja ya Addis Ababa ya kuanza kujaza maji katika bwawa hilo.
Ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha unaofanywa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile tangu mwaka 2011 umezusha mvutano mkubwa baina ya nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia.