Kwa akali watu 81 wameuawa katika mapigano Sudan Kusini
Kwa akali watu wasiopungua 81 wameuawa Sudan Kusini na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia mapigano yaliyozuka kati ya vikosi vya usalama na wanamgambo katika moja ya majimbo ya nchi hiyo.
Lul Ruai Koang, msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amethibitisha kutokea mapigano na mauaji hayo na kueleza kkwamba, mapigano hayo yametokea katika jimbo la Warrap baina ya wanamgambo wenye silaha na vikosi vya usalama katika jimbo hilo ambavyo vina jukumu la kuyapokonya silaha makundi haramu.
Afisa huyo wa jeshi la Sudan Kusini amesema kuwa, askari 55 wa serikali wameuawa katika mapigano hayo makubwa kabisa kuwahi kutokea katika miezi ya hivi karibuni na wengine 31 wamejeruhiwa.
Baadhi ya duru zinaripoti kutoka Sudan Kusini kwamba, idadi ya waliouawa katika mapigano hayo ni zaidi ya mia moja na kwamba, idadi ya majeruhi ni kubwa mno.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Aidha machafuko huko Sudan Kusini yamesababisha hali ya kibinadamu katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kuwa mbaya huku asasi mbalimbali zikionya juu ya kutokea maafa ya kibinadamu nchini humo.
Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Nchi ya Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani.