Wananchi wenye hasira wachoma moto ubalozi wa Imarati nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62847-wananchi_wenye_hasira_wachoma_moto_ubalozi_wa_imarati_nchini_libya
Wananchi wa Libya wenye hasira wamechoma moto jengo la ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) mjini Tripoli wakilalamikia hatua ya serikali ya Abu Dhabi ya kufikia makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2020 07:03 UTC
  • Wananchi wenye hasira wachoma moto ubalozi wa Imarati nchini Libya

Wananchi wa Libya wenye hasira wamechoma moto jengo la ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) mjini Tripoli wakilalamikia hatua ya serikali ya Abu Dhabi ya kufikia makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.

Taarifa zaidi kutoka nchini Libya zinasema kuwa, wananchi wenye hasira jana waliuvamia ubalozi wa Imarati mjini Tripoli na kuchoma moto sehemu ya jengo la ubalozi huo wakionyesha upinzani wao dhidi ya nchi hiyo wa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina.

Picha zilizoenezwa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na tukio hilo zinaonyesha jinsi jengo la ubalozi wa Imarati mjini Tripoli Libya lilivyoharibiwa vibaya.

Wakati huo huo malalamiko ya walimwengu yameendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya dunia dhidi ya hatua ya nchi ya Imarati ya kufikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Viongozi wa Marekani, Israel na Imarati waliofikia makubaliano ya khiana dhidi ya taifa la Palestina

Huko Afrika Mashariki pia, Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina imelaani vikali mapatano yaliyofikiwa baina ya watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel chini ya usimamizi wa makundi ya Kizayuni nchini Marekani.

Itakumbukwa kuwa, Alhamisi iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia baina ya pande mbili, hatua ambayo imeendelea kulaaniwa na kulalamikiwa katika kila kona ya dunia.