Watu 63 wafariki dunia baada ya mvua kubwa kunyesha Sudan
Viongozi wa Sudan wametangaza kuwa watu 63 wameaga dunia nchini humo baada ya kuathiriwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha mwishoni mwa mwezi Julai hadi sasa.
Idara ya Ulinzi wa Jamii imeripoti kuwa, zaidi ya nyumba na makazi elfu 14 na majengo ya serikali 119 yamebomolewa kikamilifu kutokana na mvua hizo. Mvua hizo kubwa pia zimesababisha madhara kwa nyumba nyingine 16,240.
Kwa kawaida Sudan hukumbwa na mvua kubwa kati ya miezi ya Juni na Oktoba na nchi hiyo huathiriwa na mafuriko makubwa kila mwaka.
Msemaji wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mvua kama hizi zilizonyesha mwaka jana ziliathiri maisha ya watu laki nne nchini Sudan.
Ripoti mpya ya ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan iliyotolewa Jumatano iliyopita inaeleza kuwa, maisha ya watu 185,755 wa Sudan yameathiriwa na mafuriko na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha nchini humo.