Aug 17, 2020 07:38 UTC
  • Kais Saied
    Kais Saied

Rais Kais Saied wa Tunisia ameamsha hasira za jumuiya za wanawake za kiliberali baada ya kusisitiza kwamba msingi wa mirathi katika dini ya Uislamu ni uadilifu na insafu na kwamba suala hilo limeshapewa ufumbuzi katika aya za Qu'ani tukufu ambao hauhitajii tena tafsiri wala taawili.

Kais Saied ameyasema hayo katika hafla ya Sikukuu ya Wanawake nchini Tunisia mbele ya hadhara kubwa ya jumuiya za watetezi wa haki za wanawake na kusema mzozo kuhusu urithi wa mwanamke ni mzozo usio na maana na makosa na kwamba jambo muhimu katika uwanja huo ni kuwepo usawa baina ya jinsia mbili katika haki za kiuchumi na kijamii kabla ya kujadili maudhui ya sheria za mirathi.

Rais wa Tunisia amesema kuwa aya za Qur'ani tukufu zimeweka wazi suala hilo na kwamba msingi wa mirathi katika Uislamu ni uadilifu na insafu. Amesema kuwa suala la usawa kwa mujibu wa mtazamo wa fikra za kiliberali ni la kidhahiri na kisura tu na wala halikutegemea uadilifu na insafu.

Kais Saied

Matamshi hayo ya Rais Kais Saied wa Tunisia yumkini yakazusha tena mjadala nchini humo kuhusu kadhia hiyo iliyoanzishwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Tunisia, Beji Caid Essebsi.

Tarehe 13 Agosti mwaka 2017 Caid Essebsi alipasisha pendekezo la kuwepo usawa katika mirathi baina ya mwanamke na mwanaume na kupelekwa bungeni. Hata hivyo muswada huo ulipingwa na vyama vingi katika Bunge la Tunisia na kutupiliwa mbali.

Tags