Serikali ya Sudan kutia saini mapatano ya amani na waasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62887-serikali_ya_sudan_kutia_saini_mapatano_ya_amani_na_waasi
Serikali ya Sudan itatia saini mapatano ya amani na makundi ya waasi nchini humo tarehe 28 Agosti kufuatia upatanishi na nchi jirani ya Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2020 10:07 UTC
  • Serikali ya Sudan kutia saini mapatano ya amani na waasi

Serikali ya Sudan itatia saini mapatano ya amani na makundi ya waasi nchini humo tarehe 28 Agosti kufuatia upatanishi na nchi jirani ya Sudan Kusini.

Timu ya upatanishi ya Sudan Kusini imesema pande hasimu zimeafiki kutia saini mapatano ya amani baada ya mazungumzo yaliyofanikiwa.

Mshauri wa mambo ya usalama wa rais wa Sudan Kusini na mkuu wa timu ya upatanishi Tut Gatluak amesema limebaki faili la mipango ya usalama tu kwenye ufuatiliaji wa masuala ya Darfur.

Ameongeza kuwa, wapatanishi wameweka muda ambao hautazidi siku tatu kukamilisha mafaili yote kabla ya kusainiwa makubaliano, na baadaye hatua ya mwisho ya kusaini.

Kiongozi huyo amesisitiza kwamba nchi yake ina nia ya kupatikana amani nchini Sudan.

Siku ya Jumapili iliyopita, wawakilishi wa serikali ya Sudan na kundi la waasi la SPLM linaloongozwa na Malik Agar, walisaini mapatano ya kuingizwa waasi jeshini kwa mujibu wa mapatano ya usalama katika maeneo la Kordofan Kusini na Blue Nile.

Tangu Oktoba 2019, Sudan Kusini imekuwa mpatanishi baina ya serikali ya Sudan na makundi ya waasi katika maeneo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile.

Waziri Mku wa Sudan, Abdallah Hamdok ametangaza azma ya serikali yake ya mpito kutia saini mapatano ya amani na makundi yote ya waasi nchini humo.