Chama kingine cha upinzani Sudan chapinga mwenendo wa kuanzisha uhusiano na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62969-chama_kingine_cha_upinzani_sudan_chapinga_mwenendo_wa_kuanzisha_uhusiano_na_israel
Chama cha Kimomunisti cha Sudan (Sudanese Communist Party) kimetangaza kuwa, kinapinga mpango wowote ule wa kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2020 19:33 UTC
  • Chama kingine cha upinzani Sudan chapinga mwenendo wa kuanzisha uhusiano na Israel

Chama cha Kimomunisti cha Sudan (Sudanese Communist Party) kimetangaza kuwa, kinapinga mpango wowote ule wa kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Sadiq Yousef, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho amesema: Tuko pamoja na haki za wananchi madhulumu wa Palestina katika kupinga uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa ya chama hicho imesisitiza kuwa, katu hakiungi mkono harakati za baadhi ya madola ya Kiarabu za kutaka kuanzisha uhusiano wa kidipolamasia na Israel ambayo imekuwa ikikanyanga kila leo haki za wananchi wa Palestina na kupora ardhi zao.

Msimamo huo unatangazwa siku chache tu baada ya chama kingine cha upinzani nchini Sudan cha mwanasiasa mkongwe Sadiq al-Mahdi cha The National Umma Party kulaani harakati zozote zile zenye lengo la kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na badala yake kikatoa wito wa kuungwa mkono Palestina.

Maandamano ya kupinga hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na Israel

Misimamo hiyo inatolewa katika hali ambayo, baadhi ya wanasiasa nchini Sudan wanasema kuwa, serikali ya Khartoum imekuwa ikifanya mipango ya chini kwa chini kwa ajili ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel, licha ya kuwa kidhahiri viongozi wa Khartoum wamekuwa wakilikana hilo.

Wiki iliyopita Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilimfuta kazi msemaji wake na kukanusha kauli aliyoitoa kuhusu mawasiliano kati ya Sudan na utawala bandia wa Israel kwa ajili ya kusaini makubaliano ya amani.