Polisi Uganda yazima mkutano wa upinzani, kadhaa wakamatwa
Maafisa wa polisi nchini Uganda wamezima mkutano wa kila wiki wa chama cha upinzani cha FDC na kukamata wafuasi kadhaa wa chama hicho.
Habari zinasema kuwa, Meya wa Kampala Erias Lukwago, wasomi na viongozi wa kidini ambao ni wafuasi wa chama hicho ni miongoni mwa watu waliotiwa mbaroni na polisi kwa kushiriki mkutano huo uliotajwa na vyombo vya usalama nchini humo kuwa haramu na ambao haujapata kibali cha serikali. Kadhalika waandishi wa habari waliagizwa na polisi kuondoka katika ofisi hizo za FDC katika kijiji cha Najjanankumbi, viungani mwa mji mkuu Kampala.
Hata hivyo Mkuu wa chama hicho Meja Jenerali Mugisha Muntu amewaambia waandishi wa habari kuwa wao hawababaishwi na vitisho vya polisi na kwamba mikutano na maandamano yao katika sehemu mbali mbali za nchi yataendelea kama ilivyopangwa.
Hivi karibuni, Polisi ya Uganda ilionya wafuasi wa upinzani nchini humo dhidi ya kushiriki maandamano ya Mei 5 na kusisitiza kuwa maandamano hayo hayajapata idhini ya serikali. Polisi ya Uganda kupitia naibu msemaji wake Polly Namaye imesema kuwa maandamano na mikutano hiyo ni haramu kwa kuwa inalenga kuvuruga hafla ya kuapishwa Rais Yoweri Museveni Mei 12.
Mgogoro wa kisiasa nchini Uganda uliibuka baada ya mirengo ya upinzani kupinga matokeo yaliyompa ushindi Rais Yoweri Kaguta Museveni wa nchi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Februari 18 mwaka huu.