Umoja wa Afrika wapongeza mapatano ya kihistoria ya amani Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63822-umoja_wa_afrika_wapongeza_mapatano_ya_kihistoria_ya_amani_sudan
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat amepongeza mapatano ya kihistoria ya amani baina ya makundi hasimu nchini Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2020 01:10 UTC
  • Umoja wa Afrika wapongeza mapatano ya kihistoria ya amani Sudan

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat amepongeza mapatano ya kihistoria ya amani baina ya makundi hasimu nchini Sudan.

Katika taarifa jana Jumapili, Faki alisema: "Utiwaji saini Mapatano ya Amani ya Juba ni hatua ya kihistoria kuelekea amani kwa wote nchini Sudan."

Aidha ametoa wito kwa wale ambao hawajatia saini mapatano ya amani kujiunga na mchakato wa amani. Ameongeza kuwa, Umoja wa Afrika utawasiadia wahusika wote ili kuhakikisha kuwa mapatano hayo yanatekelezwa kikamilifu.

Serikali ya Sudan pamoja na makundi makuu ya waasi, Jumamosi yalitia saini makubaliano rasmi ya kuunda serikali ya mseto na kumaliza mgogoro wa makumi ya miaka ambao umepelekea mamilioni ya watu kuwa wakimbizi na mamia ya maelfu ya wengine kuuawa.

Mwezi Agosti mwaka huu makundi matatu makuu yalitiliana saini na Sudan makubaliano ya awali ya amani, mawili ni ya jimbo la magharibi mwa nchi hiyo la Darfur na moja ni la kusini mwa nchi hiyo. Makubaliano hayo ya awali yalitiwa saini baada ya miezi mingi ya mazungumzo yaliyofanyika katika nchi jirani ya Sudan Kusini.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat

Kundi jingine kubwa la waasi la Sudan People's Liberation Movement-North (SPLMN) linaloongozwa na Abdelaziz al Hilu na ambalo halikushiriki kwenye hatua za awali za mazungumzo ya amani, nalo mwezi uliopita lilikubali kujiunga na mazungumzo ya amani yanayoendelea huko Sudan Kusini. 

Miongoni mwa vipengee vya makubaliano hayo ni kuingizwa jeshini wanamgambo waasi, kushirikishwa makundi ya waasi katika siasa na kupewa haki katika masuala ya uchumi na ardhi.