May 06, 2016 14:03 UTC
  • Hujuma ya Daesh nchini Libya yaua watu watano

Watu watano wameuawa katika shambulizi la bomu la kutegwa garini la kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika mji wa Misrata, magharibi mwa Libya.

Habari zinasema kuwa, shambulizi hilo limefanyika katika kituo cha kupekua magari karibu na eneo la Abu Qrain, yapata kilomita 80 kutoka mji wa Misrata. Mshambuliaji wa kujitolea muhanga aliyehusika kwenye hujuma hiyo ametambuliwa kwa jina la Khabab al-Tunisi, raia wa Tunisia.

Kundi hilo la kigaidi limekiri kuhusika na hujuma hiyo ya Alkhamisi na kusema kuwa limefanikiwa kudhibiti vijiji kadhaa vya mji huo pamoja na Sirte.

Hata hivyo vyanzo vingine vya habari vimesema ndege za kivita zimeshambulia maeneo ambayo yako chini ya udhibiti wa Daesh katika mji wa Misrata mapema leo na kuua magaidi wote sambamba na kuharibu magari yao.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, zaidi ya watu 20 waliuawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea katika mji wa Darnah, nchini Libya.

Libya ambayo ilitumbukia katika machafuko na ghasia baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011, katika miezi ya hivi karibuni imekuwa kwenye hali tete kutokana na kushadidi hitilafu na mapigano ya ndani kwa upande mmoja, na hujuma na mashambulizi ya makundi ya kigaidi hususan Daesh kwa upande mwingine.

Tags