Algeria na Tunisia zazuia ndege ya Israel kutumia anga zao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65359-algeria_na_tunisia_zazuia_ndege_ya_israel_kutumia_anga_zao
Algeria na Tunisia zimeizuia ndege ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuruka katika anga zao ili kuonyesha upinzani wao kwa hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2020 08:56 UTC
  • Algeria na Tunisia zazuia ndege ya Israel kutumia anga zao

Algeria na Tunisia zimeizuia ndege ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuruka katika anga zao ili kuonyesha upinzani wao kwa hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu.

Duru za habari zinaeleza kuwa, serikali za Algiers na Tunis jana Jumanne zilikataa kuruhusu ndege ya utawala huo pandikizi iliyokuwa imebeba wajumbe wa Marekani na Israel kutumia anga yake, na ndege hiyo ikalazimika kutumia njia mbadala.

Licha ya pingamizi kutoka kwa wananchi, makundi ya kiraia na wanaharakati, lakini ndege ya kwanza iliyokuwa imebeba wajumbe wa Marekani na Israel ilitua jana Jumanne katika mji mkuu wa Morocco, Rabat, baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kufuata mkumbo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Wananchi na wanaharakati nchini Morocco wamesema hatua ya kuanzisha uhusiano na utawala huo ghasibu ni tusi na jeraha kwa hisia za wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Wamorocco katika maandamano ya kupinga uhusiano na Israel

Morocco imekuwa nchi ya nne ya Kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel tokea mwezi Agosti wakati mtawala wa Marekani anayeondoka, Donald Trump alipoanzisha mkakati wa kuzishinikiza nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala huo bandia. 

Mbali na Morocco, nchi zingine za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano na Israel kwa mashinikizo ya Rais Donald Trump ni pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan.