Wapinzani Jamhuri ya Afrika ya Kati wapinga matokeo ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65614-wapinzani_jamhuri_ya_afrika_ya_kati_wapinga_matokeo_ya_uchaguzi
Wapinzani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamepinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni, wakidai ulikumbwa na dosari.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2021 04:49 UTC
  • Wapinzani Jamhuri ya Afrika ya Kati wapinga matokeo ya uchaguzi

Wapinzani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamepinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni, wakidai ulikumbwa na dosari.

Katika taarifa ya pamoja wagombea 10 wa upinzani katika uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba 27 wametaka matokeo ya uchaguzi huo yabatilishwe. Rais wa sasa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadera alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo. Siku ya Jumatatu Tume ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Touadera kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 53.92 ya kura zilizopigwa.

Endapo ushindi huo utathibitishwa na mahakama ya juu ya taifa hilo, itamaanisha kuwa hakutakuwepo duru ya pili ya upigaji kura. Hapo jana, mgombea aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 21,01, waziri mkuu wa zamani Anicet Georges Dologuele, alisema tume ya uchaguzi imechukua hatua ya kuwapuuza wapiga kura karibu laki tisa na nusu (950,000) waliozuiwa kupiga kura kutokana na ghasia za makundi yenye silaha. Mgombea aliyeshika nafasi ya tatu Martin Ziguele amesema hayapi umuhimu wowote matokeo yaliyotangazwa na tume, aliyoyataja kwa aibu kwa nchi.

 Faustin Archange Touadera

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, karibu nusu ya waliotimiza masharti ya upigaji kura, yaani watu 910,000 walijiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Desemba 27 na takriban asilimia 76.3 miongoni mwao walishiriki katika upigaji kura.Tangu alipoingia madarakani mwaka 2016 hadi sasa Rais  Faustin-Archange Touadéra amekuwa akifanya jitihada kuhakikisha maeneo mengi makubwa ya nchi hiyo yanayoshikiliwa na makundi ya wanamgambo yanarejea kwenye udhibiti wa serikali.