Mahakama ya Uganda yaiamuru polisi imuondolee Bobi Wine kizuizi cha nyumbani
(last modified Mon, 25 Jan 2021 12:42:50 GMT )
Jan 25, 2021 12:42 UTC
  • Mahakama ya Uganda yaiamuru polisi imuondolee Bobi Wine kizuizi cha nyumbani

Mahakama nchini Uganda imeamuru vikosi vya usalama vya nchi hiyo viondoe mzingiro vilioweka kwenye nyumba ya kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, ambaye yuko kwenye kizuizi cha nyumbani tangu ulipofanyika uchaguzi wa rais januari 14.

Hayo ni kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa mapema leo na wakili wa mwanasiasa huyo.

George Musisi amevieleza vyombo vya habari kuwa, serikali na vyombo vyake vinapaswa kuondoka mara moja katika eneo la nyumba ya Bobi Wine na kuhakikisha mwanasiasa huyo anarejeshewa tena uhuru wake wa binafsi.

Askari wa jeshi la polisi la Uganda wamemzuia Bobi Wine mwenye umri wa 38 kuondoka nyumbani kwake kwenye kiunga cha mji mkuu Kampala tangu baada ya kupiga kura katika uchaguzi wa Januari 14 ambapo alichuana na rais wa nchi hiyo aliyeko madarakani kwa muda mrefu, Yoweri Kaguta Museveni.

Museveni mwenye umri wa miaka 76, ambaye yuko madarakani tangu mwaka 1986, alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kujipatia asilimia 59 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Bobi Wine aliyepata asilimia 35 ya kura zote.

Rais Yoweri Museveni (kushoto) na Bobi Wine 

Bobi Wine ameyakataa matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya Uganda akidai ulifanyika udanganyifu, tuhuma ambazo serikali imezikanusha.

Mamlaka za utawala nchini Uganda zinasema, mwanasiasa huyo mkuu wa upinzani anaweza kuondoka nyumbani kwake kwenye viunga vya jiji la Kampala kwa sharti la kusindikizwa na vikosi vya jeshi kwa sababu zinahofia kujitokeza kwake hadharani kunaweza kuchochea machafuko.

Hata hivyo Jaji wa mahakama ya Uganda amesema katika hukumu yake kwamba, nyumba ya Bobi Wine si mahali mwafaka pa kumweka kizuizini mwanasiasa huyo na akazitaka mamlaka husika zimfungulie mashtaka rasmi ya uhalifu kama anahatarisha utulivu.

Msemaji wa polisi Patrick Onyango amesema hawezi kueleza chochote kwa sababu bado hawajapokea taarifa ya uamuzi huo wa mahakama.

Nayo Idara ya Mahakama ya Uganda, haijatoa taarifa yoyote kuthibitisha maelezo hayo ya wakili wa Bobi Wine.../