Machafuko ya uchaguzi yafanya laki 2 wawe wakimbizi CAR
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema watu zaidi ya 200,000 wamefurushwa au wamelazimika kuyahama makazi yao katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kutokana na machafuko ya uchaguzi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Katika kikao na waandishi wa habari jana Ijumaa mjini Geneva, Msemaji wa UNHCR, Boris Cheshirkov alisema asilimia 50 ya wakimbizi hao (laki moja) wamesalia kuwa wakimbizi wa ndani (IDPs) huku wengine zaidi ya 92 elfu wakikimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kutumia mto ulioko katika mpaka wa nchi hizo mbili.
Ameongeza kuwa, wengine 13,240 wamekimbilia usalama wao katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Jamhuri ya Congo Brazaville.
Msemaji wa UNHCR amesema makumi ya maelfu ya wakimbizi hao wanakodolewa macho na hali mbaya ya kibinadamu na wanahitaji misaada ya dharura.
Ghasia hizo za uchaguzi zilishtadi baada ya Rais Faustin-Archange Touadera wa nchi hiyo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi uliopita wa Disemba kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi wa duru moja na hivyo kukwepa kuingia katika uchaguzi mwingine. Januari 18, Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo iliidhinisha ushindi huo wa Toudera wa uchaguzi wa rais wa Disemba 27.
Muungano wa makundi ya waasi wanaobeba silaha ambao unatuhumiwa kufanya jaribio la mapinduzi ya kijeshi baada ya shambulio lao la kuvuruga zoezi la upigaji kura kufeli, umeapa kusonga mbele hadi mji mkuu wa nchi hiyo.