Bunge la Algeria lavunjwa; rais aitisha uchaguzi
(last modified Fri, 19 Feb 2021 07:07:43 GMT )
Feb 19, 2021 07:07 UTC
  • Bunge la Algeria lavunjwa; rais aitisha uchaguzi

Rais wa Algeria ameagiza kuvunjwa bunge la nchi hiyo. Rais Abdul Majid Tebboune wa Algeria jana usiku alisema kuwa amelivunja bunge ili kuendesha uchaguzi pasina ufisadi na kuandaa fursa za ajira kwa ajili ya nguvu kazi ya vijana nchini humo.

Katika taarifa yake jana usiku, Rais wa Algeria alibainisha kuwa kwa uchache hadi kufikia masaa 48 yajayo kutafanyika marekebisho katika baraza la mawaziri na matokeo yatangazwa leo Ijumaa.  

Rais Tebboune aidha ameagiza kuachiwa huru wanaharakati wa harakati ya maandamano nchini humo kwa jina la ""Hirak" protest movement".   Rais Abdul Majid Tebboune aliye na umri wa miaka 75 aliingia madarakani baada ya kufanyika uchaguzi mara baada ya kupinduliwa mtangulizi wake Abdelaziz Bouteflika kufuatia maandamano mtawalia ya wananchi ya kupinga utawala wa serikali ya rais huyo.

Rais Abdul Majid Tebboune wa Algeria  

Tebboune alikuwa Waziri Mkuu wa Algeria wakati wa utawala wa Abdelaziz Bouteflika yaani kuanzia mwezi Mei mwaka 2017 hadi alipoibuka na ushindi katika uchaguzi wa mwaka juzi.   

Awali Rais wa Algeria alieleza kuwa haridhishwi na utendaji wa serikali ya Waziri Mkuu Abdelaziz Djerad. Serikali ya Algeria inakabiliwa na changmoto mbalimbali huku janga la corona likiwa limedidimiza zaidi hali ya uchumi wa nchi hiyo.  

Wananchi wa Algeria wamekuwa wakisubiri kwa hamu utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa waliyoahidiwa baada ya kung'olewa madarani Rais Bouteflika mwaka 2019 kufuatia upinzani na maandamano yao wiki kadhaa mtawalia baada ya kusalia madarakani kwa miongo miwili.