ISIS yadai kuhusika na shambulio lililoua na kujeruhi makumi Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67862-isis_yadai_kuhusika_na_shambulio_lililoua_na_kujeruhi_makumi_nigeria
Kundi la kigaidi la ISIS tawi la Afrika Magharibi limetangaza kuhusika na shambulio dhidi ya msafara wa magari ya kijeshi lililoua na kujeruhi watu zaidi ya 30 huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 14, 2021 03:40 UTC
  • ISIS yadai kuhusika na shambulio lililoua na kujeruhi makumi Nigeria

Kundi la kigaidi la ISIS tawi la Afrika Magharibi limetangaza kuhusika na shambulio dhidi ya msafara wa magari ya kijeshi lililoua na kujeruhi watu zaidi ya 30 huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Katika taarifa, genge hilo la kigaidi limekiri kuwa ndilo lililotekeleza hujuma hiyo ya Alkhamisi iliyopita karibu na mji wa Gudumbali, eneo la Ziwa Chad, kaskazini mashariki mwa nchi.

Duru za kijeshi zinaarifu kuwa, msafara wa magari kumi ya kijeshi uliokuwa ukitokea mji wa Kukawa ukielekea Gudumbali kwa operesheni dhidi ya magenge ya kigaidi uliviziwa na kushambuliwa vikali na wanachama wa kundi hilo lenye mfungamano na Daesh.

Habari zaidi zinaarifu kuwa, raia watatu ni miongoni mwa watu 19 waliouawa katika shambulizi hilo la kundi la kigaidi la ISIS tawi la Afrika Magharibi (ISWAP).

Maafisa usalamaa wa Nigeria walishika doria

Genge hilo ambalo lilijitenga na kundi la kigaidi la Boko Haram mwaka 2016 limehusika na wimbi la mashambulio ya kigaidi nchini Nigeria hususan dhidi ya misafara ya kijeshi.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria anaendelea kukosolewa kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kuyatokomeza makundi ya kigaidi nchini humo ambayo mbali na kuua na kujeruhi maafisa usalama na raia wasio na hatia, lakini pia yanateka nyara wanafunzi kila uchao.