Mar 29, 2021 11:37 UTC
  • Jeshi la Msumbiji
    Jeshi la Msumbiji

Wizara ya Ulinzi ya Msumbiji imetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeanzisha oparesheni kubwa ya kukomboa mji wa pwani wa Palma unaodhibitiwa na kundi linalojiita al Shabab.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Msumbiji Omar Saranga amewaambia waandishi habari huko Maputo kwamba, jeshi linapambana vikali na waasi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Palma ulioko karibu na mpaka wa nchi hiyo na nchi jirani ya Tanzania. 

Mji huo ambao una akiba kubwa ya gesi inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 20, ulidhibitiwa na waasi wa al Shabab katika uvamizi uliosababisha mauaji ya makumi ya raia wasio na hatia. 

Saranga amesema jeshi la taifa la Msumbiji linafanya jitihada za kukomesha mashambulizi ya kigaidi ya kundi hilo na kurejesha amani huko Palma na kwamba, oparesheni hiyo ya jeshi imefanikiwa kuokoa maisha ya mamia ya watu wakiwemo raia wa kigeni. 

Wakati huo huo shirika la habari la Reuters limenukuu vyombo vya kidiplomasia na kiusalama kwamba, jeshi la Msumbiji halijafanikiwa bado kukomboa mji wa Palma uliodhibitiwa na waasi Ijumaa iliyopita baada ya mapigano yaliyoendelea kwa masaa 48.

Jeshi la Msumbiji, Palma

Mji wa Palma uko karibu maili sita kutoka mradi mkubwa wa gesi asili katika eneo la Afungi katika Bahari ya Hindi karibu na mpaka wa Msumbuji na Tanzania.

Habari zinasema maelfu ya raia wa mji huo wameendelea kuyakimbia makazi yao na kutafuta usalama wa roho zao mahala kwingine. 

Tags