Chama cha al Nahdha chahimiza kuanza mazungumzo ya kitaifa nchini Tunisia
Chama cha Kiislamu cha al Nahdha nchini Tunisia kimetangaza kuwa, kuna wajibu kwa wanasiasa kuanzisha mazungumzo ya kitaifa ili kupunguza mivutano katika nyuga tofauti za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Katika taarifa yake ya jana Alkhamisi, chama cha al Nahdha kimesema, Tunisia inahitajia haraka mazungumzo ya kitaifa baina ya wanasiasa kwa lengo la kuainisha vipaumbele vya kiuchumi na kijamii na kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchini hiyo.
Tamko la chama hicho limeongeza kuwa, mazungumzo ya kitaifa baina ya wanasiasa nchini Tunisia yatapunguza mizozo ya kisiasa na kijamii na yatawafanya wananchi washughulikie mustakbali wa nchi yao, suala ambalo ndilo muhimu zaidi kwao.
Baada ya wananchi wa Tunisia kufanya mapinduzi yaliyomng'oa madarakani dikteta kibaraka, Zine el Abidine Ben Ali mwaka 2011, nchi hiyo ilianza kuwa na mfumo wa Bunge na Rais mwenye nguvu na suala hilo limepelekea kuzuka mivutano mikubwa baina ya bunge na serikali huku kila mhimili kati ya mihimili hiyo muhimu ya dola ukidai kuwa na nguvu zaidi.
Rais Kais Said wa Tunisia amemteua Hichem Mechichi kuwa Waziri Mkuu na kumpa jukumu la kuunda serikali. Tarehe 16 Januari mwaka huu, Mechichi alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na kuteua mawaziri 11 wanaoiunga mkono serikali.
Hata hivyo Rais wa Tunisia amesema, mabadiliko hayo yamefanyika kinyume cha Katiba na kusema kuwa, uwezekano wa kuweko ufisadi na migongano ya maslahi ndiko kulikopelekea kufanyika mabadiliko hayo.
Mbali na mivutano hiyo ya kubadilisha mfumo wa zamani wa utawala, wananchi wa Tunisia bado wanateseka kwa matatizo ya kiuchumi na hawaridhishwi na viongozi wanaoingia madarakani.