Serikali ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati yajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71132-serikali_ya_waziri_mkuu_wa_jamhuri_ya_afrika_ya_kati_yajiuzulu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Firmin Ngrébada ametangaza kujiuzulu yeye pamoja na serikali yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2021 03:20 UTC
  • Serikali ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati yajiuzulu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Firmin Ngrébada ametangaza kujiuzulu yeye pamoja na serikali yake.

Katika ujumbe aliouandika jana Alkhamisi kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Waziri Mkuu huyo wa CAR amesema, "Nimeshakabidhi barua yangu ya kujiuzulu pamoja na serikali yangu kwa Rais Faustin Archange Touadera."

Farmin hata hivyo hajatoa maelezo zaidi kuhusu uamuzi wake huo wa kuachia ngazi yeye pamoja na serikali aliyokuwa akiiongoza.

Hii ni katika hali ambayo, Jumanne iliyopita ya Juni 8, shirika la habari la Associated Press lilinukuu ripoti ya Mei 31 ya kituo cha 'Global Center for the Responsibility to Protect' iliyosema kuwa, magenge ya watu wanaobeba silaha yangali yanadhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya CAR, huku yakivuna faida kutokana na utozaji ushuru haramu na magendo ya silaha.

Ripoti hiyo ilisema, wingu la kutoheshimiwa sheria limechochea zaidi ghasia zinazoshuhudia sasa nchini humo, na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na magenge yanayobeba silaha pamoja na maafisa usalama wa serikali.

Ghasia zilivyosababisha mgogoro wa wakimbizi CAR

Tayari Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshalaani uvunjaji huo wa haki za binadamu na wimbi la kuuawa askari wa kulinda amani wa umoja huo katika nchi hiyo ya katikati mwa bara Afrika.

Mapema mwaka huu, genge la waasi liliua wanajeshi wawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA), siku chache tu baada ya askari mwingine wa Umoja wa Mataifa kutoka Burundi kuuawa nchini humo.