Wahajiri 17 wapoteza maisha katika fukwe za Tunisia
Shirika la Hilal Nyekundu la Tunisia limetangaza kuwa, wahajiri 17 wamekufa maji katika fukwe za nchi hiyo baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka baharini.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Reuters ambalo limenukuu taarifa ya Hilal Nyekundu ya Tunisia ikisema jana kuwa, wahajiri hao walikusudia kuelekea Libya na baadaye Italia, kabla ya mtumwi wao kupinduka na kusababisha vifo vya wahajiri wasiopungua 17.
Shirika la Hilal Nyekundu la Tunisia limetangaza pia kuwa, gadi ya ulinzi wa ufukweni ya nchi hiyo imefanikiwa kuokoa wahajiri 380.
Wahajiri wengi waliokuwemo kwenye mtumbwi huo ni kutoka nchi za Syria, Misri, Sudan, Eritrea, Mali na Bangladesh na umepinduka katika eneo la kaskazini magharibi mwa Libya.
Mwaka 2020 wahajiri 90 wa nchi za Afrika walikufa maji katika juhudi za kuvuka Bahari ya Mediterranean kuelekea Ulaya. Ajali hiyo ilihesabiwa kuwa moja ya ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea katika eneo hilo.
Kila wiki Gadi ya Ufukweni ya Tunisia inaokoa wahajiri wengi wanaopanda kwenye mitumbwi dhaifu kujaribu kuvuka mawimbi makali ya bahari kubwa wa Mediterranean. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, idadi ya mitumbwi inayobeba wahajiri kuwapeleka Ulaya imeongezeka sana. Vituo vya kupokelea wakimbizi vimejaa kupindukia huko Tunisia na idadi ya wahajiri wanaofariki dunia kwa sababu mbalimbali imeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni.