Chama cha Ennahdha chamtaka Rais wa Tunisia kutengua maamuzi yake
Chama cha Ennahdha kimemtaka Rais wa Tunisia atengue maamuzi aliyochukua hivi karibuni ya kumfuta kazi waziri mkuu na kusitisha shughuli za Bunge la nchi hiyo.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, chama hicho kimesema, Rais Kais Saied wa Tunisia anapaswa kufuta maamuzi yake ya karibuni na kutatua changamoto zilizopo kwa kutumia katiba.
Chama hicho pia kimetoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kuiondoa Tunisia katika mgogoro wa sasa.
Jumapili iliyopita Rais Kais Saied wa Tunisia alichukua hatua ya kushtukiza ya kumfuta kazi Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hichem Mechichi na kulivunja Bunge. Rais wa Tunisia amehalalisha maamuzi aliyochukua siku ya Jumapili na kudai kuwa amechukua maamuzi hayo ili kurejesha utulivu na kuinusuru Tunisia.
Wapinzani wanasema Rais huyo wa Tunisia amefanya mapinduzi baridi akishirikiana na jeshi la nchi hiyo. Kambi ya upinzani imewataka wananchi wapinge uamuzi huo kwa kufanya maandamano kote nchini Tunisia.
Katika upande mwingine, Rais wa Tunisia ametoa dikrii akipiga marufuku kutembea wakati wa usiku kwa muda wa mwezi mmoja. Vilevile amepiga marufuku mijumuiko ya watu zaidi ya watatu katika barabara kuu nchini Tunisia.
Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kutatuliwa hitilafu zilizojitokeza huko Tunisia kupitia njia ya mazungumzo.