UN yaiomba Kenya isifunge kambi za wakimbizi Wasomali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7435-un_yaiomba_kenya_isifunge_kambi_za_wakimbizi_wasomali
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Ijumaa amekutana na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini Nairobi kujadili uamuzi wa nchi yake kuwatimua wakimbizi kutoka Somalia walioko katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ya Dadaab.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2016 11:55 UTC
  • UN yaiomba Kenya isifunge kambi za wakimbizi Wasomali

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Ijumaa amekutana na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini Nairobi kujadili uamuzi wa nchi yake kuwatimua wakimbizi kutoka Somalia walioko katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ya Dadaab.

Mabalozi hao wa nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama wameelekea Nairobi siku chache tu baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kumpigia simu Rais Kenyatta akimuomba kutofunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Rais mjini Nairobi imesema kadhia ya kufungwa kambi hiyo imejadiliwa kwa urefu katika kikao hicho. Aidha katika kikao hicho, kumejadiliwa pia hali jumla nchini Somalia na kazi za Kikosi cha Umoja wa Afrika cha Kulinda Amani Somalia AMISOM ambacho kinajumuisha askari kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Djibouti, Ethiopia na Sierra Leone.

Kenya imesema sababu kuu ya kutaka kufunga kambi ya wakimbizi wa Daadab ni kuwa tishio kwa usalama wa nchi hiyo kutokana na magaidi wa Al Shabaab kuchanganyika na wakimbizi.

Baada ya kukutana na ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa Rais Kenyatta amerejea eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya linalopakana na Somalia kuendelea na safari yake ya kukagua miradi ya maendeleo na hali ya usalama katika eneo hilo ambalo pia limekuwa likilengwa na magaidi wa Al Shabaab.