Wanajeshi Sudan waendelea kukabiliana na waandamanaji; vurugu zatawala
Vyombo vya usalama nchini Sudan vimeendelea kupambana na waandamanaji wenye hasira wanaoipinga mapinduzi ya kijeshi ya Jumatatu iliyopita ambayo yamezidi kuzorotesha kipindi cha mpito cha kidemokrasia, na kusababisha ukosolewaji mkubwa kieneo na kimataifa.
Takriban waandamanaji wanne wameripotiwa kuuawa hiyo jana kwa mujibu wa maafisa wa afya katika siku ya nne mfululizo ambapo ghasia zinaendelea katika mitaa na barabara za jiji la Khartoum.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kuuawa waandamanaji wanne hapo jana kunaifanya idadi ya waandamanaji waliouwawa tangu Jumatatu yalipotokea mapinduzi kufikia 7 na wengine zaidi 170 kujeruhiwa. Hata hivyo duru za kujitegemea zinasema kuwa, idadi ya waliouawa katika maandamano hayo ni zaidi ya hiyo iliyotangazwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa kauli moja uamuzi wa kupinga na kulaani mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan na kutoa wito wa kurejeshwa utawala wa kiraia nchini humo sambamba na kuachiliwa huru viongozi wote wanaoshikiliwa kizuizini.
Jumatatu iliyopita ya tarehe 25 Oktoba majenerali wa jeshi la Sudan walifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Mapinduzi hayo ya kijeshi yalifanyika chini ya mwezi mmoja tu kabla ya muda aliopaswa Jenerali al Burhan kukabidhi uongozi wa Baraza la Utawala linaloendesha nchi, kwa viongozi wa kiraia, hatua ambayo ingelipunguza nguvu za jeshi za kushikilia madaraka.