Mkutano wa Paris wataka askari wa kigeni walioivamia Libya waondoke nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i76860-mkutano_wa_paris_wataka_askari_wa_kigeni_walioivamia_libya_waondoke_nchini_humo
Washiriki wa mkutano wa Paris, mji mkuu wa Ufaransa wametaka kufanyike uchaguzi katika tarehe iliyopangwa nchini Libya, kama ambavyo wamehimiza pia wajibu wa kutoka wanajeshi wa kigeni nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2021 08:06 UTC
  • Mkutano wa Paris wataka askari wa kigeni walioivamia Libya waondoke nchini humo

Washiriki wa mkutano wa Paris, mji mkuu wa Ufaransa wametaka kufanyike uchaguzi katika tarehe iliyopangwa nchini Libya, kama ambavyo wamehimiza pia wajibu wa kutoka wanajeshi wa kigeni nchini humo.

Televisheni ya France 24 imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, viongozi wa nchi 30 walioshiriki kwenye mkutano wa Paris kuzungumzia masuala ya Libya wamesema kuwa, watamuwekea vikwazo yoyote atakayefanya njama za kukwamisha uchaguzi wa rais na bunge nchini Libya katika tarehe iliyopangwa ya Disemba 24 mwaka huu.

Walioshiriki kwenye mkutano huo akiwemo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamezitaka nchi kama Uturuki kuondoa wanajeshi wao walioko Libya haraka iwezekanavyo.

Waziri Mkuu wa Libya na Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huo. Waziri Mkuu wa nchi hiyo ameahidi kukabidhi madaraka kwa mtu yeyote atakayechaguliwa na wananchi, lakini kwa sharti uchaguzi huo ufanyike kwa amani na kushirikisha pande zote.

Jeshi la Uturuki nchini Libya

 

Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita, Rais wa Algeria alitangaza kuwa, hatashiriki mkutano wa Paris ulioitishwa kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa nchini Libya.

Juzi Alkhamisi, shirika la habari la Reuters lilinukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Algeria ikitangaza kwamba, itatuma mwakilishi tu kushiriki katika mkutano wa Kimataifa wa Libya uliofanyika jana Ijumaa.

Hatua hiyo ya Algiers imechukuliwa huku uhusiano wa pande hizo mbili ukiendelea kuyumba baada ya matamshi ya kifidhuli ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuhusu historia ya Algeria ambaye alidai kuwa kabla ya wakoloni wa Ufaransa kuivamia nchi hiyo, hakukuwa kabisa na taifa liitwalo Algeria.